Kuwa na Wema na Moyo Mpana

Ninaomba maisha yenu yajazwe upendo na baraka za Mungu. Sasa ningependa kushiriki nanyi neema kupitia ujumbe wenye kichwa “Wema na Moyo Mpana.” 

Mtu mwenye moyo mpana na mpole hufananishwa na bahari. Bahari hukusanya maji ya kila aina kutoka mito, mabonde na vijito, hata maji machafu, kisha huyasafisha. Ukikuza moyo mpana na mpole kama bahari, unaweza kuiongoza njia ya wokovu nafsi ya aina yoyote iliyochafuliwa na dhambi. 

Moyo mpole hukumbatia kila mtu na wengi hupata pumziko ndani yake. Ukiwa mpole moyoni na mwema katika mwenendo wako, utazigusa nafsi za watu wengi zaidi na kutimiza kazi kubwa zaidi za Mungu kwa uwezo mkubwa. Unapaswa kufanya nini ili kuwa na upole na wema? Kwanza, ondoa uovu na utakaswe. 

Unapoondoa mizizi ya uovu na kuwa bila lawama katika maneno, matendo na mwenendo wako, watu wengi wanaweza kukujia na kupata pumziko. Kwa hiyo, kupitia Neno la Mungu na maombi ya bidii, chunguza matendo madogo ya mwili na uyabadilishe yawe kweli kwa mwongozo wa Roho Mtakatifu. 

Baadhi yenu mara nyingi hufanya mizaha na marafiki au wakati mwingine kusema maneno yasiyofaa bila nia mbaya. Wengine hawavai kwa unadhifu wala hawajali mavazi yao. Ingawa mambo haya huonekana madogo, ukikamilika katika matendo madogo pamoja na kuwa mpole moyoni, utaaminika, kupendwa na kuheshimiwa kuwa mtu mwenye adabu. 

Pili, ili kuwa mwema, unapaswa kuukuza moyo wako uwe mzuri. Tabia ya moyo inahusu ukubwa wa chombo cha moyo. Kwa kutegemea tabia ya moyo, wengine hufanya zaidi ya wanavyoweza, wengine hutimiza tu walichokabidhiwa, na wengine hushindwa kutimiza wajibu wao. 

Mtu mwema ana moyo mpana na mkubwa kiasi cha kufanya zaidi ya anavyotarajiwa. Tabia hii ya moyo hutofautiana kulingana na jinsi unavyoupanua katika kila hali, kwa hiyo unaweza kuibadili kwa juhudi zisizokoma. Huenda awali ulikuwa na mawazo finyu na kujali mambo yako tu, lakini unapoomba na kupokea msaada wa Roho Mtakatifu, moyo wako hupanuka na kuanza kujali mambo na hali za wengine. 

Kwa hiyo, ninaomba katika jina la Bwana Yesu kwamba muukuze moyo wenu uwe mpole na usio na lawama, na muupanue ili muweze kuongoza na kutunza shirika kubwa lenye watu wa aina mbalimbali!

    Askofu Mstaafu, Dkt. Jaerock Lee

Neno la Uzima