Uwe Hodari na Moyo Mkuu

Andiko: 1 Yohana 3:21–22: “Wapenzi, mioyo yetu isipotuhukumu, tuna ujasiri kwa Mungu; na lo lote tuombalo, twalipokea kwake, kwa kuwa twazishika amri zake, na kuyatenda yapendezayo machoni pake.”

Ninaomba maisha yenu yajazwe upendo na baraka za Mungu, na ningependa kushiriki nanyi neema kupitia ujumbe wenye kichwa “Uwe Hodari na Moyo Mkuu.”

Watu wa dunia huona mtu kuwa hodari na jasiri anapokuwa mkaidi, mwepesi wa kugombana na kutimiza wajibu wake bila kusalimu amri. Lakini mbele za Mungu, kuwa hodari na jasiri kuna maana tofauti. Ukiwa mpole na mnyenyekevu, lakini ukapambana bila hofu na adui Ibilisi na kumshinda katika vita vya kiroho, na ukamwomba Mungu kwa ujasiri na kupokea, unaweza kuitwa hodari na jasiri machoni pa Mungu. Basi, ufanye nini ili uwe hodari na jasiri mbele za Mungu? Kwanza kabisa, utahiri moyo wako.

Mungu alimwamuru Abrahamu kutahiriwa kwa mara ya kwanza, na Waisraeli walitahiriwa siku ya nane baada ya kuzaliwa. Leo pia tunapaswa kutahiriwa, lakini si katika mwili bali moyoni, kwa kuwa tunaishi katika enzi ya Roho Mtakatifu. Kutahiri moyo kunamaanisha kukata ngozi ya moyo; unapolishika Neno la Mungu, kuondoa dhambi na kuishi katika kweli, unaweza kuutahiri moyo wako.

Kwa maneno mengine, moyo hutahiriwa unapoondoa kila aina ya uongo, uovu, ukosefu wa haki, uasi wa sheria na giza vinavyopingana na Neno la Mungu, na kutakaswa. Je, wakati mwingine unahisi utupu na uzito moyoni ingawa umetimiza wajibu wako, kulitumikia kanisa na kuhudhuria ibada na mikutano kwa ukawaida? Ikiwa ndivyo, huenda inaonyesha kwamba umeacha kuutahiri moyo wako na umesimama palepale katika ukuaji wa kiroho.

Kwa mfano, huenda usionekane kuwa na kiburi katika maneno na matendo yako, lakini ndani ukatamani kuhudumiwa. Tuseme unafanya biashara bila kuvunja sheria wala kumdanganya mtu, lakini bado unatamani kupata faida kwa njia isiyofaa. Ikiwa hujafanya dhambi hizo waziwazi, huenda bado hujajitahidi kung’oa kabisa asili hizo za dhambi kupitia maombi ya bidii na kufunga.

Unaweza kuzitubia kwa muda, lakini ukaendelea kuficha mizizi ya dhambi hizo. Hivyo, huna ujasiri mbele za Mungu na unaonekana kukosa moyo mkuu. Unaweza kujazwa Roho Mtakatifu na kuwa hodari na jasiri unapoendelea kuutahiri moyo wako na kutimiza moyo wa kiroho uliotakaswa kwa njia hiyo.

Kama 1 Yohana 3:21–22 inavyosema, “Wapenzi, mioyo yetu isipotuhukumu, tuna ujasiri kwa Mungu; na lo lote tuombalo, twalipokea kwake, kwa kuwa twazishika amri zake, na kuyatenda yapendezayo machoni pake,” ninaomba kila mmoja wenu awe hodari na jasiri mbele za Mungu, apokee kila alichoomba na amtukuze Mungu. Ninaomba haya katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo!

    His Emeritus Bishop Dr. Jaerock Lee

Word of Life