Utakatifu

Andiko: Mithali 22:11: “Ampendaye moyo safi, na mwenye neema ya midomo, mfalme huwa rafiki yake.” Ninaomba maisha yenu yajazwe upendo na baraka za Mungu. Leo ningependa kushiriki nanyi neema kupitia ujumbe wenye kichwa “Utakatifu.”

Neno “mtakatifu” humhusu tu yule asiye na dhambi kabisa, kwa hiyo halina uhusiano na wanadamu. Linafaa kumwelezea Mungu wetu, ambaye ndiye wema wenyewe. Hata hivyo, 1 Petro 1:15–16 inasema, “Lakini kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote; kwa maana imeandikwa, Mtakuwa watakatifu kwa kuwa mimi ni mtakatifu.” Tufanye nini ili tuwe watakatifu kama Mungu wetu anavyotaka? Kwanza, takaswa kutoka moyoni, si kwa nje tu. Mungu anataka uutakase moyo wako. Kwa maneno mengine, anataka uikate ngozi ya moyo na kuutahiri, ili ubadilike uwe mwema na safi bila uovu wowote.

Watu humhukumu mwingine kwa kuangalia sura yake tu, lakini Mungu huutazama moyo wa kila mmoja. Ndiyo maana ukiwa na wivu, chuki, malalamiko na mambo kama hayo moyoni, Mungu hawezi kukuona kuwa mtu wa kumcha. Haimaanishi kwamba huhitaji kujali mwonekano wako mradi tu uwe na moyo safi.

Ukiutakasa moyo wako, utakuwa nadhifu katika mwonekano na matendo yako daima, iwe wengine wanakuona au la. Kama Mithali 22:11 inavyosema, “Ampendaye moyo safi, na mwenye neema ya midomo, mfalme huwa rafiki yake,” utasema maneno mema na mazuri. Kama vile maji na mafuta yasivyoweza kuchanganyika, moyo wako ukiwa safi utaishi maisha yaliyotengwa na dunia. Pili, ili utakaswe, usifurahie mambo ya kidunia bali mambo ya kumcha Mungu.

Unapaswa kutamani ulimwengu mzuri wa kiroho, kujifunza Neno la Mungu na kuomba. Pia tamani kwa furaha kufanya kazi zozote za Mungu. Ukiwa na moyo huo, utatamani thawabu za mbinguni na kutimiza kwa hiari wajibu uliopewa na Mungu kwa ajili ya Ufalme wake.

Tatu, ili utakaswe, unapaswa kuwa mnyenyekevu na kujishusha. Usipoteze moyo wako wa kwanza, bali uendelee kuuboresha. Uwe tayari kumpa Mungu mengi zaidi kuliko hapo awali na kujitoa kwa hiari zaidi. Ukijitukuza na kusema, “Nimefikia cheo hiki na nimependelewa kiasi hiki,” huwezi kamwe kuonekana kuwa na moyo safi.

Kwa hiyo, ninaomba kadiri Mungu anavyokupendelea, ndivyo unyenyekevu wako unavyozidi kuongezeka. Ninaomba kila mmoja wenu aimbe sifa kwa Mungu Baba yetu na kumtukuza milele, na pia awe mtu mwenye heshima mbinguni. Ninaomba haya katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo!

    His Emeritus Bishop Dr. Jaerock Lee

Word of Life