Maisha Yasiyo na Majuto

Ninaomba maisha yenu yajazwe upendo na baraka za Mungu. Sasa ningependa kushiriki nanyi neema kupitia ujumbe wenye kichwa “Maisha Yasiyo na Majuto.” Kila mtu hupewa uhai mara moja tu.

Wanapotazama nyuma na kutafakari maisha yao ya zamani, watu wengi hawawezi kusema kwamba wameishi maisha yenye thamani ya kweli; badala yake hujuta na kujiuliza, “Kwa nini nilifanya hivyo?” Sulemani, mfalme wa tatu wa Israeli, aliustawisha ufalme wake na kufurahia utajiri, heshima na umaarufu mkubwa kwa baraka za Mungu. Pia alipata hekima ambayo haikuwa imewahi kupewa mtu mwingine, akajikusanyia maarifa mengi, akajenga majumba ya kifahari na kujitwalia masuria wengi warembo kama alivyotaka.

Lakini mwishoni mwa maisha yake alilazimika kukiri, “Ubatili mtupu! Ubatili mtupu! Yote ni ubatili.” Kwa kuwa wanadamu wameumbwa kwa mfano wa Mungu, wana hamu ya umilele na hivyo hawawezi kuridhika kikamilifu na mambo ya mwili. Kukiri kwa mwisho kwa Mfalme Sulemani kunatufundisha jambo hili. Haidhuru umepata tuzo na heshima kiasi gani duniani, usipopokea wokovu na uzima wa milele, utakachoweza kufanya mbele ya Hukumu Kuu ni kujuta.

Ni maisha ya aina gani yanayoweza kuitwa maisha yasiyo na majuto? Kwanza, unaweza kuishi bila majuto unapokimbia mashindano ya imani ukiwa na upendo mkuu kwa Mungu. Ikiwa umeuelewa kweli upendo wa Mungu, hutasita kumkabidhi kila ulicho nacho anapokuomba. Badala yake, hata baada ya kufanya hivyo utatafakari ni kitu gani kingine zaidi unachoweza kumpa. Mtume Paulo aliacha kila kitu alichokuwa nacho, zikiwemo familia, maarifa, heshima na utajiri, akamchagua Mungu.

Kwa hiyo, kwa kibali cha Mungu akawa mtume wa nguvu na wa Neno la kiroho la Mungu, naye akaandaliwa thawabu tukufu katika Ufalme wa Mbinguni. Pili, unapaswa kuukuza na kuukamilisha moyo wako ili uishi bila majuto. Ili kuukamilisha moyo wako, ondoa kila aina ya uovu na dhambi na uujaze kweli. Moyo mkamilifu huonekana katika maneno unayosema. Moyo wako ukijaa kweli, kinywa chako kitasema kweli pekee. Moyo safi huufanya mdomo wako pia kuwa safi.

Mwisho, unaweza kuishi bila majuto unapokuwa na amani na watu wote. Kwa hiyo, ondoa tabia ya kuwabagua wengine na tamaa zote za kutafuta faida yako mwenyewe; badala yake, jiweke katika nafasi ya wengine. Ukiwa umeondoa kila aina ya uovu na kuufanya moyo wako kuwa mkamilifu, unaweza kuwa na amani na kila mtu. Ninaomba uishi maisha yenye thamani na uzuri, yasiyo na majuto kweli duniani, na wakati wa mwisho wa maisha yako uweze kusema kwamba ulijitahidi kadiri uwezavyo.

Ninaomba katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo kwamba Mungu atambue safari yako yote ya maisha, na kwamba kwa ujasiri ujikabidhi mikononi mwa Bwana na kupokea thawabu tukufu mbinguni.

    His Emeritus Bishop Dr. Jaerock Lee

Word of Life