Moyo Mwema wa Yonathani

Ninaomba maisha yenu yajazwe upendo na baraka za Mungu. Sasa ningependa kushiriki nanyi neema kupitia ujumbe wenye kichwa “Moyo Mwema wa Yonathani.” Yonathani alikuwa mwana wa kwanza wa Sauli, mfalme wa kwanza wa Israeli.

Ilitarajiwa kwamba Yonathani angeketi kwenye kiti cha enzi baada ya Sauli. Lakini Mungu alimtia mafuta Daudi kuwa mfalme ajaye wa Israeli. Kwa mtazamo wa kibinadamu, Daudi alikuwa mpinzani au adui wa Yonathani. Hata hivyo, Yonathani alimpenda Daudi kama maisha yake mwenyewe. Hili liliwezekana kwa sababu Yonathani alikuwa na moyo mwema. Basi, alikuwa na wema wa aina gani?

Kwanza, Yonathani alifuata mapenzi ya Mungu bila kutafuta faida yake mwenyewe. Aliambiwa kwamba Mungu alikuwa amemtia mafuta Daudi kuwa mfalme ajaye kwa sababu baba yake Sauli alikuwa ametenda uovu mwingi mbele za Mungu. Yonathani alipokea habari hiyo bila kulalamika wala kuwa na hisia mbaya; badala yake, alimsaidia Daudi kwa hiari apate kiti cha enzi. Alikuwa tayari kuachia heshima na utukufu wake ili mapenzi ya Mungu yatimizwe.

Pili, Yonathani alijitahidi kadiri awezavyo kumzuia mwingine asitende dhambi. Daudi alipookoa nchi katika vita dhidi ya Wafilisti, Waisraeli wengi walimsifu na kumpendelea. Lakini Mfalme Sauli alimwonea wivu sana na baadaye akawatuma askari nyumbani kwa Daudi ili wamuue. Yonathani alijua kwamba huenda angeumizwa akimkabili baba yake Sauli, lakini alimjia kwa ujasiri na kujaribu kumshauri kuhusu matendo yake mabaya. Ukiwahukumu na kuwasengenya vibaya viongozi wako kwa sababu maoni yao hayapatani na yako, inaonyesha kwamba huna wema wala upendo.

Pia, huwezi kuitwa mwema ukiepuka viongozi wako wanapotenda dhambi na kupotoka. Ukikaa kimya kwa sababu ni vigumu kumshauri kiongozi wako au unaogopa atakudhuru, hutimizi wajibu wako kama mwanadamu na jambo hilo si sawa machoni pa Mungu. Zaidi ya yote, unapaswa kuwa na ujasiri wa kumwambia kiongozi wako kweli, na wakati huohuo umshauri kwa wema, upendo na moyo wa kumtumikia bila kumuumiza.

Mwisho, Yonathani alitimiza wajibu wake kama mwana kwa Sauli hadi dakika za mwisho. Mtu mwenye moyo mwema anaweza kuhuzunika anapomwona mtu akitenda uovu, na kutotaka kukaa karibu na watu waovu. Lakini Yonathani aliutimiza wajibu wake wa mwana kwa baba yake Sauli licha ya maumivu aliyopitia kwa sababu yake. Alibaki pamoja na baba yake hadi alipokufa vitani.

Simaanishi kwamba ni wema kukaa na mtu mwovu hadi mwisho. Yonathani alijua uovu wa baba yake Sauli na mara kadhaa alimshauri asitende dhambi tena. Lakini hakuweza kumgeuzia baba yake kisogo, kwa hiyo alibaki kando yake.

Hata hivyo, hakushiriki kamwe katika matendo maovu ya Sauli. Kwa hiyo, iga wema wa Yonathani, aliyefuata mapenzi ya Mungu bila kutafuta faida yake mwenyewe na kujitahidi kumzuia baba yake asitende dhambi; takaswa kabisa ili upokee baraka ambazo Mungu ameandaa. Ninaomba haya katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo!

    His Emeritus Bishop Dr. Jaerock Lee

Word of Life