Kuwa Rafiki wa Mfalme

Mungu wetu ni Nuru, wala ndani yake hamna giza lolote. Hana lawama wala doa; ni mtakatifu na mkamilifu. Yeyote anayependa usafi wa moyo hupambana na dhambi na kuzitupilia mbali hata ikibidi kumwaga damu, na huondoa kila namna ya uovu.

Mithali 22:11 inasema, “Ampendaye moyo safi, na mwenye neema ya midomo, mfalme huwa rafiki yake.” Mstari huu unafunua siri ya kuwa rafiki wa mfalme wa nchi: kupenda usafi wa moyo na kusema maneno yenye neema. Mtu huonekana kuwa mwenye neema anapowakumbatia na kuwatia moyo wengine kwa unyenyekevu unaotoka moyoni.

Mtu wa namna hiyo hawakwazi wengine, hatizami kasoro zao, wala hawahukumu au kuwalaumu. Badala yake, huwaelewa na kuwakubali wengine, ili aweze kuwaongoza watu wengi kadiri iwezekanavyo katika njia ya kweli. Vivyo hivyo, mtu mwenye neema ya kweli hukuza moyoni wema wote, haki na ukweli, na huzaa matunda ya Nuru katika matendo na maneno yake.

Kwa hiyo, huonekana kuwa mwaminifu na hupendwa na watu wote; popote aendapo, huleta uzima. Kwa maneno mengine, huwapa suluhisho linalopatana na Neno la Mungu wale wanaokabiliwa na matatizo na majaribu mbalimbali. Pia hutimiza wajibu wake kama mwanadamu, hukuza uaminifu na kudumu katika Neno la Mungu, ili maneno na matendo yake ya kweli yawe mfano mwema na furaha kwa wengine. Kama Mungu asemavyo katika 1 Wathesalonike 4:3, “Maana haya ndiyo mapenzi ya Mungu, kutakaswa kwenu,” anataka watoto wake wawe watakatifu.

Mtu anayependa usafi wa moyo hushikilia kweli katika hali zote na husema maneno yanayowajenga na kuwapa neema wanaoyasikia. Yusufu, mwana wa Yakobo, alikuwa na moyo huo wenye neema. Alipouzwa utumwani Misri, bwana wake alimwamini na kumpendelea. Hata alipokuwa gerezani, walinzi walimtambua na kumweka kuwa msimamizi wa wafungwa wengine wote.

Mwishowe, Farao alivutiwa na hekima na maneno yake yenye neema, akamteua kuwa mtawala wa nchi ya Misri, wa pili baada ya Farao. Ninaomba kila mmoja wenu autakase moyo wake na kusema maneno yenye neema pekee, ili kumpendeza Mungu wetu na kuishi maisha yenye baraka na utukufu. Ninaomba haya katika jina la Bwana wetu!

    His Emeritus Bishop Dr. Jaerock Lee

Word of Life