Amani

Andiko: Mithali 1:33: “Bali anisikilizaye atakaa salama, naye atatulia bila kuogopa mabaya.” Ninaomba maisha yenu yajazwe upendo na baraka za Mungu. Sasa ningependa kushiriki nanyi neema kupitia ujumbe wenye kichwa “Amani.”

Ukiulizwa ni sura ya nani inayoonekana kuwa na amani zaidi, wengi wenu mtajibu ni ya mtoto anayelala kifuani mwa mama yake. Watu wanataka kuweka chini mizigo na mahangaiko yao ya kila aina na kutumaini kuishi maisha ya amani kama mtoto huyo, lakini si rahisi.

Basi, ufanye nini ili ufurahie amani ya kweli moyoni? Yesu alituahidi katika Yohana 14:27 akisema, “Amani nawaachieni; amani yangu nawapa; niwapavyo mimi sivyo kama ulimwengu utoavyo. Msifadhaike mioyoni mwenu, wala msiwe na woga.” Kwa hiyo, amani ya kweli hutoka kwa Baba aliye juu pekee kupitia neema ya Bwana wetu Yesu Kristo.

Hata hivyo, ukikiri kuwa na imani kwa Mungu lakini usipoishi katika kweli, huwezi kufurahia amani ya kweli moyoni. Usipoondoa moyoni chuki, ugomvi, wivu, kiburi, hasira ya haraka na majivuno, utapoteza amani ya moyo. Kwa mfano, ukisikia neno linalokudharau, unaweza kuumia kwa sababu ya majivuno, moyo wako ukafadhaika na chuki ikachochewa. Unapowaona watu wanaoonekana duni kuliko wewe wakiishi maisha bora zaidi, moyo wako unaweza kuvurugika na kutoridhika kwa sababu ya wivu.

Kisha utavunjika moyo na kupoteza hamu ya kufanya jambo muhimu. Kadiri unavyokuwa na mambo mengi yasiyo ya kweli moyoni mwako, ndivyo amani ya kweli inavyopungua. Amani huja tu unapoyaondoa mambo ya mwili moyoni na kuujaza tumaini la mbinguni na Neno la kweli la Mungu.

Ikiwa umeondoa kabisa kiburi na hasira ya haraka, haidhuru ni nani anayekusema vibaya au kukusumbua, hutajisikia vibaya wala kulemewa. Hata ukikaripiwa kwa ukosefu wa haki na bila sababu, utatafakari maisha yako ya zamani tena na kumtabasamia mwenzako kwa uchangamfu.

Kwa hiyo, hata kama bado hujatakaswa kikamilifu, ukiishi maisha yanayofaa ya imani na kuondoa moyoni mwako mambo yasiyo ya kweli moja baada ya jingine, furaha kutoka kwa Baba aliye juu na tumaini la mbinguni vitaujaza moyo wako, na uso wako utang’aa kwa nuru ya kiroho. Hivyo ndivyo unavyoweza kufurahia amani ya kweli. Kwa hiyo, ninakusihi kwa maombi uondoe uovu na dhambi upesi na kuubadilisha moyo wako uwe wa kweli, ili ufurahie amani na faraja ya kweli.

Katika Mithali 1:33 Mungu anasema, “Bali anisikilizaye atakaa salama, naye atatulia bila kuogopa mabaya.” Ninaomba Mungu awabariki katika kila jambo mnalofanya na kuijaza mioyo yenu furaha na amani ya mbinguni. Ninaomba haya katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo!

    His Emeritus Bishop Dr. Jaerock Lee

Word of Life