Andiko la Biblia la leo: Kutoka 20:4–6
“Usijifanyie sanamu ya kuchonga, wala mfano wa kitu chochote kilicho juu mbinguni, kilicho chini duniani, wala kilicho majini chini ya dunia. Usivisujudie wala kuvitumikia; kwa kuwa mimi, Bwana, Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu, nawapatiliza wana maovu ya baba zao, hata kizazi cha tatu na cha nne cha wanichukiao; nami nawarehemu maelfu elfu wanipendao na kuzishika amri zangu.”
Ndugu wapendwa, leo ni kipindi cha pili cha mfululizo wa Amri Kumi.
Wiki iliyopita tulijifunza Amri ya Kwanza, isemayo tusiwe na miungu mingine ila Mungu pekee. Mungu wa pekee ndiye aliyeumba wanadamu na kila kitu kilichopo; huwapa wanadamu uhai na baraka. Watu wanapotumikia sanamu zisizo na maana, yaani miungu mingine, huteswa na adui Ibilisi na Shetani. Mungu wetu mwenye upendo aliweka Amri ya Kwanza ili tupate ulinzi na baraka kwa kumtumikia yeye pekee.
Leo tutajifunza Amri ya Pili inayokataza kuabudu sanamu. Hatupaswi kujitengenezea sanamu wala kuabudu sanamu za namna yoyote. Lakini amri hii haimaanishi tu kutokuabudu sanamu tulizotengeneza kwa mikono yetu. Sikilizeni ujumbe huu na mtafakari kama mmeabudu sanamu kiroho, hata kama mnaamini kwamba mmemtumikia Mungu pekee. Ninaomba katika jina la Bwana muondoe sanamu zote maishani mwenu na kuwa watoto wapendwa na waliobarikiwa wa Mungu.